Wananchi wengi wa Tanzania wameendelea kuishi katika maumivu na hofu kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa uchaguzi. Katika sakata hilo, watu walipigwa, walikamatwa na vyombo vya usalama, huku wengine wakifunguliwa kesi nzito zikiwemo za uhaini, na baadhi yao bado wakiwa mahabusu hadi sasa.
Ripoti kutoka kwa mashuhuda na wanaharakati wa haki za binadamu zinaeleza kuwa baadhi ya waliokamatwa walichukuliwa kwa nguvu wakati wa maandamano ya kupinga mwenendo wa uchaguzi, huku familia zao zikikosa taarifa rasmi kuhusu waliko au hali zao.
Kutokana na hali hiyo, makundi ya kiraia na wadau wa haki za binadamu wanatarajiwa kudai haki na uwajibikaji , wakitaka waliofungwa kuachiliwa au kusikilizwa kwa haki, na uchunguzi huru kufanyika kuhusu mateso yaliyotokea.
Wito unaendelea kutolewa kwa serikali kuheshimu haki za binadamu, kulinda amani, na kuhakikisha haki inapatikana kwa waathirika wote wa vurugu za kisiasa.